Friday, October 26, 2012

Coca Cola India shutumani

Kampuni ya vinywaji baridi ya Coca Cola India italazimika kufikiria upya mpango wake wa kupanua uzalishaji kutokana na shutuma nyingi kwamba inasababisha uharibifu wa mazingira ikiwemo kupunguza kiwango cha maji ardhini.

Ikiwa ndio mzalishaji mkubwa wa soda nchini India, Coca Cola imekuwa ikizidi kulaumiwa kuwa shughuli zake zilizotarajiwa kuzalisha ajira na kuinua uchumi wa wakazi wa maeneo ya karibu na viwanda vyake, zimegeuka hatari kwa maisha ya watu.

Viongozi wa kampuni hiyo sasa wanakibarua kizito cha kuthibitishia ulimwengu kuwa shughuli zake haziathiri mazingira bali zaidi zimelenga kuleta maendeleo kwa pande zote za maisha.

Mwaka jana, Coca Cola India ilitangaza kuwa itatumia Dola 500 milioni kuongeza kufikia mwaka 2020 baada ya kugundua soko kubwa la bidhaa zake.

Mkurugenzi Mtendaji wake, Muhtar Kent anasema: "Tunaamini kuna soko kubwa hapa na tunalenga kulipata kwa kuwa wananchi wa India wanashauku kubwa ya kutumia vinywaji tunavyozalisha. Ni soko ambalo halijafuatiliwa ipasavyo."

Mipango hiyo na kauli za wamiliki wa Coca Cola nchini India ni tofauti na zilivyo fikra za wananchi kwani wanaona kuwa shughuli za kampuni hiyo zimeanza kuhatarisha hatima ya maelfu ya watu wanaotegemea kilimo kwa kusababisha uhaba mkubwa wa maji na kuharibu rutba ardhini.

Maji machafu yaliyochanganyika na kemikali zinazotokana na shughuli za uzalishaji za Coca Cola hupenya na kusambaa hadi kwenye visima ambavyo maji yake yanategemewa sana na wananchi kwa matumizi ya majumbani na mashambani.

Matatizo makubwa yanayotajwa kusumbua wananchi ni matumizi ya kemikali, kiasi kikubwa cha maji na malighafi inayotumika kuhifadhia viwanyaji.

Matatizo ya kiafya yanayokabili wananchi hao yanatokana na kuwepo kwa asidi (tindikali) kwenye baadhi ya bidhaa za Coca Cola hivyo kusababisha kuozesha meno, hasahasa kwa watoto.

Kituo cha Sayansi na Mazingira (CSE) ambacho ni shirika la kiraia jijini New Delhi, kimebainisha kuwa maji machafu yanayotokana na uzalishaji wa soda nchini India, yana aina mbalimbali za sumu na kuzitaja baadhi kama lindane, DDT na malathion.

Kemikali hizo zinaweza kusababisha magonjwa ya kensa (saratani) pamoja na kupungua kwa nguvu ya mfumo wa kupambana na wadudu mwilini.

Kituo hicho kimechunguza vinywaji kama Coke, Pepsi pamoja na 7Up, Mirinda, Fanta, Thums Up, Limca na Sprite, vingi vikiwa vinatengenezwa na Coca Cola.

Kituo cha Radio 4 katika kipindi chake "Pata Ukweli" au "Face the Facts" kimetoa kwa mara ya kwanza taarifa nyingi za jinsi kemikali zinazotumiwa kutengeneza vinywaji hivyo zinavyozalisha sumu inayotapakaa hadi kwenye kingo za mito.

Kituo hicho kimefichua uchunguzi uliofanywa na Chuo Kikuu cha Exeter uliobainisha kuwepo kwa chembechembe za sumu zinazoweza kuathiri mifumo ya hisia ya watoto.

Pia baadhi ya chembechembe hizo hufyonzwa na mimea (ikijumuisha mazao ya mboga) hivyo kuweza kuathiri figo, ini na kusababisha kensa.

Mwanasayansi David Santillo anasema kuwepo kwa chembechembe za kemikali hizo kwa muda mrefu kwenye ardhi zinazotumika kwa kilimo, kunahatarisha afya za wanadamu watakapotumia mazao ya kilimo.

Katika jimbo la Kerala, kusini mwa India, tayari matatizo yameanza kuwapata wanavijiji kadhaa ambao wanatatizwa na uhaba mkubwa wa maji kiasi cha Coca Cola kuanza kuwasambazia maelfu ya lita za maji safi kila asubuhi.

Matumizi makubwa ya maji katika utengenezaji wa bidhaa zake, yameanza kuathiri kilimo na tayari serikali ya eneo hilo imeamua kufuta leseni ya kampuni hiyo.

Mtaalamu wa mazingira nchini India, Vandana Shiva anasema mpango wa Coca Cola kupanua uzalishaji, utakuwa na athari kubwa kwa wananchi kwani utengenezaji wa lita moja tu ya soda ya Coke, huhitaji lita tisa za maji safi.

Kampuni hiyo pia inalaumiwa kwa kuzuia ushindani, kutoa rushwa kwa madaktari ili wasitoe taarifa sahihi za athari za afya na mazingira, mauaji yanayofanywa na vikosi vya walinzi wake na unyanyasaji kazini.

Japokuwa Coca Cola nchini India inaendelea kushughulikia kesi kadhaa mahakamani yenyewe ikizuia vikwazo vya kuendelea na biashara, shurti irudi na kuangalia upya mipango yake ya maendeleo.

No comments:

Post a Comment